Monday , 7th Jul , 2014

Waziri kivuli wa maliasili na utalii mchungaji Peter Msigwa ameonesha mkanda wa video na kuanika kile alichookiita kuwa ni uozo na ukiukwaji mkubwa wa sheria ya wanyama pori unaofanywa kupitia vitalu vya uwindaji.

Waziri Kivuli wa Maliasili na utalii, Mchungaji Peter Msigwa.

Akizungumza jijini Dar es salaam, mchungaji Msigwa amefichua namna moja ya makampuni yaliyopewa leseni ya uwindaji ya Green miles Safaris, ambayo ina kitalu katika mbuga ya Selous, ilivyovunja sheria kwa kuwaua wanyama wadogo, kufanya ukatili wakati wa kuwakamata na hata kukiuka hata sheria za kimataifa ambazo Tanzania kama nchi imeziridhia.

Kwa mujibu wa Mchungaji Msigwa, ukiukwaji mkubwa wa sheria unaofanywa na makampuni ya uwindaji yanatia shaka hata umiliki wake na kutolea mfano utata wa umililiki unavyoighubika kampuni ya Green Miles Safaris kutokana na baadhi ya vielelezo amedai vinaonesha kampuni hiyo inamilikiwa na mzawa wakati sio hivyo.

Mchungaji Msigwa amemtaka waziri wa maliasili na utalii Lazaro Nyalandu kuwawajibisha watendaji wote katika idara ya wanyamapori sambamba na kuchukua hatua kali dhidi ya kampuni ya Green Miles Safaris ikiwa pamoja na kuifutia kampuni hiyo leseni ya uwindaji.

Hatua nyingine ambazo waziri huyo kivuli wa maliasili na utalii amependekeza zichukuliwe ni pamoja na kuharakishwa kwa uchunguzi wa kimahakama kuhusu operesheni TOKOMEZA ambayo amesema itafichua mambo mengine yaliyojificha na ambayo Watanzania wa kawaida hawawezi kuyafahamu ikiwa ni pamoja na namna wamiliki wa kampuni za uwindaji wanavyoongoza kwa ujangili na uwindaji haramu.