Friday , 15th Jan , 2016

Watu 48 wanaodaiwa kuwa ni wahamiaji haramu mkoani Morogoro wamefukuzwa nchini na wengine wamefikishwa mahakamani kwa kuingia nchini na kufanya kazi kinyume cha sheria.

Hayo yamebainishwa na Naibu Kamishna wa Uhamiaji wa Mkoa wa Morogoro, Agustino Haule, alipokuwa akielezea hatua mbalimbali zinazochukuliwa na idara hiyo katika hatua ya kukabiliana na wimbi la wahamiaji haramu.

Amesema wahamiaji haramu kutoka mataifa mbalimbali wamepatikana katika msako uliofanyika maeneo mbalimbali ikiwemo viwandani, shuleni, majumbani na katika taasisi mbalimbali zilizopo mkoani Morogoro. Ametaja wahamiaji haramu hao ni kutoka katika nchi za Kenya, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Aidha Operesheni ya kuwasaka wahamiaji haramu nchini ilitangazwa na wizara ya mambo ya ndani na idara ya uhamiaji inatekeleza agizo hilo katika maeneo yote nchini.