Wednesday , 1st Jun , 2016

Serikali imesema kuwa takribani Kaya elfu 25,446 ziliingia kwa udanganyifu kwenye mradi wa TASAF kutokana na kukosa sifa za kuwa na kiwango cha umasikini ikiwemo baadhi ya viongozi wa Kaya kuwaingiza ndugu zao katika mradi huo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. George Simbachawene.

Akiongea leo Bunge katika kipindi cha Maswali na Majibu Waziri wa Nchi Ofisi ya rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. George Simbachawene, amesema kuwa serikali imeanza kuchukua hatua juu ya watumishi waliohusika katika udanganyifu ambapo baadhi ya sehemu umefanywa kwa makusudi.

Mhe. Simbachawene amesema kuwa hatua za haraka walizozifanya kama serikali ni kuziondoa Kaya zote zilizoorodheshwa kama kaya masikini na kuendelea kufanya utafiti kaya wa kuzibaini kaya zinazolengwa kwa ajili ya kupitiwa na mradi huo.

Mhe. Simbachawene amesema kuwa katika zoezi hilo tafiti zilizofanywa zinaonyesha mkoa wa Kigoma unaongoza kwa Kaya nyingi kufanya udanganyifu ambapo ni zaidi ya elfu moja na kusema hatua ambazo zitachukuliwa katika mkoa huo ndio zitakazochukuliwa sehemu nyingine.

Akizungumzia kuhusu kuongeza kiwango cha fedha hizo baada baadhi ya wanufaika wa mradi huo kusema ni kidogo amesema kuwa serikali imefanya tafiti na kuona kiasi hicho kinatosha kujikwamua endapo wanufaika watatumia fedha hizo ipasavyo.