Thursday , 14th Jul , 2016

Kampuni nne za usafirishaji wa abiria na mizigo nchini zimetozwa faini zaidi ya shilingi Milioni 73 kwa makosa mbalimbali ya kukiuka taratibu na sheria ya mazingira ya mwaka 2004 ya usafi wa mazingira.

Miongoni mwa mambo yaliyobainika ni pamoja na kutiririsha maji yenye kemikali kwenye makazi ya watu mtaa wa Jumuiya B wilaya ya Temeke.

Akizungumza na wananchi ambao ni waathirika wa maji taka hayo Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mheshimiwa Luhaga Mpina amesema serikali imebaini baadhi ya wafanyabiashara nchini wamekuwa wakikiuka maagizo ya serikali kwa makusudi hivyo wameanza kuwafikisha mahakamani wafanyabiashara wote wanaokiuka sheria za mazingira.

Kwa upande wake mratibu wa mazingira Kanda ya Mashariki bwana Jaffari Chimgege amesema pesa zote zinazolipwa ikiwa ni faini za mazingira zinaingizwa kwenye mfuko wa maendeleo nchini.

Chimgege amesema faini zote zinatakiwa zilipwe ndani ya siku saba na kama hazikulipwa kwa muda huo uliotolewa viwanda hivyo vitafungiwa visitoe huduma hizo kabisa.