Wednesday , 4th Feb , 2015

Mabweni matatu ya shule ya sekondari Engutoto wilayani Monduli mkoani Arusha yameteketea kwa moto usiku wa kuamikia leo na kuunguza vitu vyote yakiwemo madaftari nguo na vitabu.

Mabweni matatu ya shule ya sekondari Engutoto wilayani Monduli mkoani Arusha yameteketea kwa moto usiku wa kuamikia leo na kuunguza vitu vyote yakiwemo madaftari nguo na vitabu huku vifaa vingine vikitajwa kuibwa na baadhi ya watu waliokuwa wanawaokoa wanafunzi hao.

Wakizungumza shuleni hapo wanafunzi walionusurika na tukio hilo wamesema tukio limetokea wakati wanafunzi hao wakiwa katika masomo ya usiku.

Wamesema kwamba moto huo umeteketeza kila kitu hawana nguo wala vifaa vya shule na wengine wanafanya mtihani mwaka huu hivyo wameiomba serikali na wadau wawasaidie ili kuendelea na masomo.
 
Mkuu wa shule ya sekondari Engutoto Lomaiyan Sailep amesema hali ni mbaya hasa ukizingatia tukio hili limetokea ghafla lakini walimu na wadau wengine wanafanya mpango wa kutatua tatizo hilo.
 
Naye mkuu wa wilaya ya Monduli Jowika Kasunga amesema pamoja na kuwa tatizo ilo ni kubwa na la kusikitisha lakini binadamu wamekosa utu kwani baadhi ya watu wameiba vifaa vya wanafunzi na kukimbia navyo lakini serikali itahakikisha inawatafuta watu hao sambamba na kutafuta ufumbuzi ili watoto waendelee kusoma.