Thursday , 26th Jul , 2018

Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Mkoa wa Manyara, Chelestino Mofuga leo amesimamia shughuli ya kuteketezwa kwa moto kwa nyumba sita wilayani humo kwa kukaidi agizo la serikali la kuondoka ndani ya siku saba katika maeneo ya Hifadhi ya Bonde la Yaeda Chini.

Mofuga amesema njia hiyo itasaidia kulinda hifadhi hiyo na kuongeza kuwa, operesheni ya kuwaondoa wavamizi hao kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na Jeshi la Polisi, baada ya watu hao kuchomewa nyumba zao watachukuliwa hatua za kisheria ikiwamo kupelekwa mahakamani.

Awali alipotembelea katika hifadhi hiyo Mofuga alitoa siku saba kwa wavamizi kuondoka kwa hiari vinginevyo wataondolewa kwa nguvu.

Mofuga alisema hayupo tayari kuona watu wakiharibu mazingira ya bonde hilo, kwamba wanatakiwa kuondoka na kuacha shughuli zote wanazozifanya.

Wakati anatoa agizo hilo, Mofuga alisema kwamba wananchi hao wanapaswa kutambua umuhimu wa kuhifadhi mazingira kwa ajili ya hifadhi kwa manufaa ya kizazi kilichopo na kijacho.

Miongoni mwa nyumba zilizoteketezwa kwa moto ni pamoja na ya Diwani wa Kata ya Eshkesh, Rumay Ologa ambaye baada ya kupata taarifa hizo alijisalimisha Kituo cha Polisi cha Hydom.