Saturday , 5th Dec , 2015

Rais Mstaafu wa awamu ya tatu nchini Tanzania Mhe. Benjamin William Mkapa, amewataka wazazi wa mikoa ya Kusini mwa Tanzania kutoa msukumo kwa watoto wao kujali umuhimu wa elimu, ili wanufaike na uwekezaji unaoendelea katika mikoa hiyo.

Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, awamu ya tatu, Benjamin William mkapa akihutubia katika moja na mikutano aliyoaalikwa

Rais Mstaafu wa awamu ya tatu nchini Tanzania Mhe. Benjamin William Mkapa, amewataka wazazi wa mikoa ya Kusini mwa Tanzania kutoa msukumo kwa watoto wao kujali umuhimu wa elimu, ili wanufaike na uwekezaji unaoendelea katika mikoa hiyo unaotokana na rasilimali za gesi na mafuta.

Akizungumza mkoani Mtwara katika Mahafali ya nne ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Stella Maris, amesema kumekuwa na msukumo mdogo kwa wazazi katika kusisitiza umuhimu wa elimu kwa vijana wa mikoa hiyo, jambo ambalo linapelekea kuwa na uhaba wa vijana wanaopata elimu ya juu katika vyuo vilivyopo nchini.

Mkapa amesema anasikitishwa na takwimu za matokeo ya mitihani kwa shule za sekondari za miaka ya karibuni kwa mikoa ya Kusini na Pwani, kutokana na shule kutofanya vizuri kwenye mitihani yao na kuhathiri hata udahili wa wanafunzi katika taasisi mbalimbali.

Awali mkuu wa chuo hicho, Slaus Mwisomba, amesema chuo hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa maabara kwa ajili ya masomo ya Sayansi ambayo ni Fizikia, Kemia na Baiolojia.