Rais mstaafu wa awamu ya tatu nchini Tanzania, Mhe. Benjamin William Mkapa,
Rais mstaafu wa awamu ya tatu nchini Tanzania, Mhe. Benjamin William Mkapa, ameelezea kusikitishwa na jinsi Tanzania pamoja na nchi nyingine za Afrika Mashariki, zilivyosaini mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi, baina ya Jumuiya ya Ulaya na nchi za Afrika, Karibeani na Pasifiki, mkataba unaojulikana kwa kifupi kama EPA (Economic Partnership Agreement).
Akizungumza na watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Mkapa ameutaja mkataba huo kuwa ni aina nyingine ya ukoloni kama ilivyokuwa kwa mkataba wa Berlin wa mwaka 1880, ambapo nchi za Ulaya zililigawa bara la Afrika kwa ajili ya manufaa yao kiuchumi.
Amesema kupitia mkataba huo, ni vigumu kwa kampuni za kiafrika kushinda zabuni katika nchi za Ulaya lakini ni rahisi kwa kampuni za Ulaya kushinda zabuni katika nchi za Afrika kutokana na kukomaa kiteknolojia, na hata zinaposhindanishwa kampuni za Afrika na Ulaya ni rahisi kwa kampuni za Ulaya kushinda, jambo litakalochangia kuua kampuni za kiafrika
Mhe. Benjamin William Mkapa, amewataka watumishi wa wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa kuwa wazalendo linapokuja suala la kujadili masuala mbali mbali yanayohusu maslahi ya nchi.
Mkapa amesema dhana ya uzalendo ni muhimu kwa watumishi hao hasa nchi inaposaini makubaliano mbalimbali ya kimataifa.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernard Membe, amesema kusainiwa kwa mkataba huo ni matokeo ya kukosekana kwa ushirikiano baina ya wizara yake katika mikataba ya kimataifa, ambapo ameahidi kuonana na Spika wa Bunge Bi. Anne Makinda kwa lengo la kuwasihi wabunge wasiridhie mkataba huo alioutaja kuwa ni wa kinyonyaji.