Tuesday , 28th May , 2019

Zaidi ya wanafunzi wa kike 5000, wanatarajiwa kupatiwa taulo za kike kwa mwaka mzima ili kuwasaidia kuendelea na majukumu yao kama kawaida ikiwemo kuhudhuria masomo pindi wanapokuwa katika kipindi cha hedhi.

Mkuu wa Vipindi wa East Africa Radio, Nasser Kingu.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Vipindi wa East Africa Radio, Nasser Kingu, wakati akimzungumza katika  uzinduzi wa Kampeni ya NAMTHAMINI, ambayo huendeshwa na East Africa Television Limited, ikiwa ni mwaka wa tatu mfululizo.

Kingu amesema kuwa Kwa mwaka 2019, Namthamini inatarajia kufikia Mikoa ya   Dar es salaam, Arusha, Mbeya, Mwanza, Dodoma, Pwani, Mara, Kigoma , Manyara, Tabora, Morogoro na Njombe. Lakini pia mbali na ugawaji wa taulo za kike itatolewa elimu juu ya hedhi salama, na masuala mazima ya hedhi.

"Kampeni hii imezinduliwa leo Mei 28, 2019 ikiwa ni siku ya hedhi Duniani na itaendelea kufanyika kwa kipindi cha mwaka mzima (ikiwa na siku maalumu kila mwezi), ili kuweza kumwezesha binti huyu kufikia malengo kwa kutokukosa masomo yake awapo katika siku zake kwa sababu ya ukosefu wa taulo hizi", amesema Kingu.

Kwa mwaka  2017, Namthamini ilifanikiwa kufikia takribani wanafunzi 550, ndani ya mikoa 5 nchini ikiwa ni robo ya lengo lililokuwa limewekwa kuweza kuwapatia taulo watakazotumia kwa mwaka mzima, na kwa mwaka 2018 ilifanikiwa kufikia wanafunzi 2773, na wote walipatiwa taulo za kuweza kutumia kwa mwaka mzima wakiwa mashuleni.

Kwa makampuni, taasisi na Watanzania wanaweza kuchangia kampeni ya Namthamini kwa kupeleka mahitaji kama taulo za kike (Pad) moja kwa moja ofisi za East Africa Television zilizopo Mikocheni Dar es salaam.

Pili ni kwa kutuma pesa katika akaunti ya Namthamini kwenye benki ya CRDB/ 0150431938200 au kwa Airtel Money namba - 0787 633 313 East Africa Television.

Bofya hapo chini kutazama namna uzinduzi wa Namthamini ulivyofanyika.