Wednesday , 21st Jan , 2015

Madereva wa daladala jijini  Arusha wamegoma  kutoa  huduma  za  usafiri  kwa  zaidi  saa  sita  wakiwalalamikia  vituo vipya  vya  kupakia  na  kushusha  abiria  vilivyowekwa  na  mamlaka  za  usafirishaji .

Vituo hivyo vipya ni hatua  inayolenga  kupunguza  tatizo  la foleni  linaloendelea  kulikabili  jiji  hilo  siku  hadi  siku.  

Wakizungumzia mgomo  huo  ambao ulisababisha  adha kubwa  kwa wananchi   madereva hao  ambao  kulingana  na  utaratibu  mpya  hawataruhusiwa   kuanzia  safari   katikati  ya  jiji,  wamesema  hauna tija  kwao  na   wana wasiwasi  kuwa  hizo ni njama  za  kuwaondoa katika  eneo hilo.

Mwenyeki wa chama cha wasafirishaji   wa  abiria  mkoa  wa  Arusha  Adolfu  Loken  amesema malalamiko  ya madereva hao  hayana  msingi  kwani  utaratibu huo  umezingatia  mahitaji  ya  pande  zote  na  ndio  suluhisho  la  tatizo  la  msongamo linaloendelea  kuathiri  sekta  hiyo.

Hali hiyo imezua vurugu zilizoambatana na makundi ya vijana wapiga debe kuvunja vioo vya magari ambayo yalikuwa yamekaidi msimamo wa mgomo na kusababisha askari wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) kuingilia kati kuwatawanya.

Mamia ya abiria, wakiwemo wanafunzi na wafanyabiashara, leo wamelazimika kutembea kwa miguu na wengine kukodi pikipiki maarufu kama bodaboda.

Kutokana na mgogoro huo, maafisa wa halmashauri ya jiji la Arusha, Chama cha Wasafirishaji na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa nchi Kavu na Majani (SUMATRA) wamekutana kwa dharura ambapo baada ya kikao, wameazimiakuwa utaratibu mpya kuendelea.