Mganga Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita akizungumza na EATV muda mfupi baada ya kukabidhi vifaa tiba kwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Baadhi ya vifaa vilivyotolewa ni pamoja na mashine kumi za kupimia mapigo ya moyo, pampu maalumu mbili, vipima joto 110, mashine sita za kupimia uzito za aina ya springi na nyingine sita ambazo mtoto hupimwa akiwa amelala.
Mkurugenzi Mtendaji wa mgodi huo Bw. Terry Mulpeter amesema msaada huo ni moja ya mipango ya mgodi huo ya kuhakikisha kuwa unakuwa sehemu ya jamii na uwepo wa wake unaleta manufaa kwa jamii inayouzunguka.
"GGM inatoa msaada huu kwa kuzingatia kwamba mahitaji ya vifaa hivi ni makubwa na kwa sababu ya uhaba wa bajeti mara nyingi hospitali zetu zimeshindwa kukidhi manunuzi ya vifaa hivi muhimu, hivyo basi GGM kama mdau katika sekta ya Afya, imeamua kuchangia ili watoto na kina mama watakaofika hospitalini hapo waweze pata huduma hizi muhimu," amesema Bw. Mulpeter
Kwa upande wake, Meneja Mawasiliano na Mahusiano kwa Umma wa mgodi huo Bw. Tenga B. Tenga amesema GGM imekuwa ikitoa huduma mbalimbali za afya nchini ikiwa ni pamoja na Kufanya ukarabati mkubwa wa hospitali teule ya Geita ambapo takribani Shilling billion moja za Kitanzania zimewekezwa katika hospitali hiyo.
Huduma nyingine ni ile ya matibabu ya watu wenye matatizo ya midomo sungura inayofanyika kila mwaka ambapo zaidi ya watu elfu moja wamekwishapatiwa huduma hiyo kwa udhamini wa mgodi sambamba na zoezi la kila mwaka la upulizaji wa dawa za kuzuia mbu wanaoeneza ugonjwa wa malaria katika Mji wa Geita.
Aidha, ametaja huduma nyingine ni kampeni ijulikanayo kama Kili Challenge, ambapo mgodi ukishirikiana na wadau mbali mbali pamoja na Tume ya Kudhibiti Ukimwi TACAIDS, umekuwa ukipandisha watu Mlima Kilimanjaro ili kuchangisha fedha ambazo baadaye huelekezwa katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi.
"Hali kadhalika GGM imejenga vituo kadhaa vya matibabu katika mji wa Geita, Nyakabale na Buhongo hospitali iliyoko kwenye Meli ya Vine Trust inayosimamiwa na Kanisal la African Inland Church, ni moja ya huduma nyingine ambapo Mgodi umewekeza shilingi milioni 600, ili kuwezesha meli hiyo kufikia zaidi ya wakazi laki nne na nusu wanaozunguka ziwa Victoria," amesema Bw. Tenga.