Mbunge wa jimbo la Mtwara mjini (CUF) Maftaha Nachuma
Wakizungumza wakati wa kujiandikisha kwa ajili ya kuanza masomo katika programu hiyo inayofahamika kama Maftaha English Leaning Program, baadhi yao wamesema wameshawishika kujiunga kwasababu wanaamini ukosefu wa ajira wanaokabiliana nao kwa sasa ni kutokana na kutokuwa na elimu ya kutosha ikiwa ni pamoja na kutojua lugha ya kiingereza.
Kwa upande wake, mbunge huyo amesema alibaini kuwepo kwa changamoto hiyo kutokana na kuzunguka katika ofisi na kampuni mbalimbali za serikali na watu binafsi ambapo aligundua uhaba wa wananchi wa Kusini walioajiriwa katika ofisi hizo huku alipouliza sababu za uhaba wao alijibiwa kuwa wananchi wengi hawana elimu.
Aidha, amesema amefurahishwa na muitikio wa watu ambao ni zaidi ya 500 walijitokeza kujiandikisha huku akiwataka wananchi hao wazidi kujituma ili waweze kufikia malengo kwasababu kusoma hakuna umri, ambapo amesema mpango huo anaugharamia mwenyewe kupitia mshahara wake na tayari walimu wameshapatikana kwa ajili ya kuanza kufundisha.