Saturday , 17th Sep , 2016

Katibu tawala wa Mkoa wa Singida Dkt Angelina M. Lutambi leo ameupokea Mwenge wa Uhuru ambao utakimbizwa Mkoani Singida kwa siku saba na kuhusika katika uzinduzi wa Miradi 33 yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 14.

Dkt. Lutambi amekabidhiwa Mwenge huo pamoja na wakimbiza Mwenge Kitaifa katika eneo la Kijiji cha Lusilile Kata ya Kintinku Wilaya ya Manyoni ambapo amesema kuwa mwenge wa Uhuru ukiwa Mkoani humo utapitia jumla ya miradi 61 inayohusu sekta ya ufugaji, Mazingira, Afya, Elimu, Barabara, Utawala Bora, Kilimo, pamoja na Programu za mapambano dhidi ya Dawa za kulevya.

Mbio za Mwenge wa uhuru ambazo zimebeba kauli mbiu ya "Vijana ni nguvu kazi ya Taifa, Washirikishwe na kuwezeshwa" ambapo kila Halamashauri nchini zimeelekezwa kutenga asilimia 5% ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya vijana na asilimia 5% nyingine kwa ajili ya kuwawezesha akina mama wajasiriamali.

Akikabidhi mwenge huo katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Bi. Rehema Madenge amesema kuwa Mwenge wa Uhuru umekimbizwa katika Wilaya zote saba za Mkoa huo ambapo jumla ya Miradi 47 yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 12 na kuwapongeza wananchi wote kwa ushirikiano na juhudi kubwa walizofanya katika kuianzisha, kuiendeleza na kuikamilisha Miradi yote.

Miongoni mwa Miradi itakayofunguliwa ni pamoja na uzinduzi wa Programu ya Ufuatiliaji na kuteketeza mbu, Kufungua Mradi wa ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na matundu nane ya vyoo na ukarabati wa vyumba viwili vya madarasa, Ufunguzi wa daraja la Makutupora, Kuzindua Klabu ya wapinga Rushwa, Kuzindua Mradi wa Ujenzi wa kituo cha Maarifa ya kupambana na UKIMWI, Kuzindua Mradi wa Vijana wa kufyatua matofali, na Kuzindua Klabu ya Kupambana na Dawa za Kulevya.

Kwa mujibu wa ratiba za mbio za Mwenge wa Uhuru za mwaka huu, unakimbizwa katika Halmashauri na Manispaa zipatazo 179 na kilele cha mbio hizo ni Octoba 14 mwaka huu katika Mkoa wa Simiyu.