Monday , 15th Feb , 2016

Serikali nchini Tanzania imesema imeanza majadiliano na kuangalia changamoto zinazozikabili nchi za ukanda wa maziwa makuu kuhusu utekelezaji wa ujenzi wa reli itakayotumika kusafirishia bidhaa katika nchi hizo.

Akizungumza mara baada ya mkutano uliowakutanisha Waziri wa Uchukuzi na Miundombinu kutoka nchi Tano za ukanda huo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema changamoto mojawapo ilikuwa ni vizuizi 15 vya barabarani.

Prof. Mbarawa amesema ujenzi wa reli ya kati utainufaisha zaidi Tanzania katika nchi za ukanda huo kutokana na asilimia 90 ya reli kuwapo nchini ambapo kati ya Kilometa 2600, kilometa 1500 zipo nchini.

Prof, Mbarawa ameongeza kuwa kukamilika kwa reli hiyo ambayo inatarajiwa kuanza kujengwa na kukamilika ndani ya miaka mitano itawanufaisha wananchi na kuongeza kwa ajira.

Kwa upande wake mwenyekiti wa mawaziri wa nchi hizo ambaye ni waziri wa miundombinu wa Rwanda, James Musoni amesema hali ya miundombinu katika ukanda huo inahitaji kufanyiwa marekebisho makubwa.