Saturday , 19th Dec , 2015

Maafisa elimu wa Halmashauri za Masasi na Nanyumbu mkoani Mtwara wametakiwa kuinua viwango vya ufaulu katika halmashauri zao kutokana na kushika nafasi mbili za mwisho kimkoa katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba.

Wanafunzi wa Shule za Msingi nchini Tanzania wanaokabiliwa na ukosefu wa madawati wakiwa wamekaa chini darasani.

Maafisa elimu wa Halmashauri za Masasi na Nanyumbu mkoani Mtwara wametakiwa kuinua viwango vya ufaulu katika halmashauri zao kutokana na kushika nafasi mbili za mwisho kimkoa katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba.

Akizungumza mkoani humo katika kikao cha uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga na kidato cha kwanza mwaka 2016, katibu tawala wa mkoa huo, Alferd Luanda, amesema hii ni mara ya mwisho kwa maafisa elimu hao kutoa matokeo mabaya na iwapo hawatapandisha ufaulu watachukuliwa hatua.

Akitolea maelezo sababu za kufanya vibaya katika halmashauri yake, mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Nanyumbu, Idris Mtande, amesema sababu kubwa ni wazazi kukosa muitikio mzuri kielimu na ukosefu wa vitendea kazi ikiwa ni pamoja magari katika idara ya elimu.

Mkoa wa Mtwara umeshika nafasi ya 12 kitaifa katika matokeo ya mtihani huo na kurudi nyuma kwa nafasi mbili baada ya mwaka jana kuwa katika nafasi ya 10, huku halmashauri ya Mtwara vijijini ikiwa ya kwanza kimkoa kwa kufaulisha kwa asilimia 86.84 ikifuatiwa na halmashauri ya manispaa ya Mtwara yenye asilimia 77.8, ambapo jumla ya wanafunzi 15,670 mkoani humo wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika mwaka ujao.