Mkuu wa mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Stephen Kebwe
Akiwa katika ziara ya kazi Mkoani humo Mkuu huyo wa Mkoa amekutana na kamati ya kusuluhisha migogoro baina ya wafugaji wa kimasai na wamang’ati wanaoibiana mifugo huku akiagiza kuondolewa mara moja wafugaji wote walioingia katika Mkoa wa Morogoro kuondoka kabla ya operesheni kabambe haijaanza.
Dkt. Kebwe amesema kuwa marufuku hiyo itaendelea kwa muda wakati serikali ikiendelea na zoezi la kuweka mipaka ya kudumu kwa kuanza na wilaya ya Mvomero ambayo ndio inatatizo kubwa la migogoro kati ya wafugaji na wakulima.
Nao wafugaji wa kijiji cha Ngerengere wameiomba serikali kuwatengea maeneo ya kutosha kwa ajili ya malisho yatakayosaidia kupunguza msuguano baina ya wakulima na wafugaji katika maeneo mengi ya mkoa wa Morogoro.
Katika hatua nyingine kikosi cha kuzuia ujangili kikishirikiana na wakala wa huduma za misitu Wilaya ya Mvomero wamefanya operesheni na kukamata ng’ombe zaidi ya 900 walioingizwa kwenye msitu wa hifadhi ya Morogoro kinyume cha sheria.
Meneja msaidizi wa misitu wilaya hiyo Bw. Sulemani Burenga amewataka wafugaji kuacha uvunjaji wa sheria kwa kuendelea kuvamia maeneo ya hifadhi.