Wednesday , 12th Dec , 2018

Serikali imepiga marufuku uchomaji matofali kwa njia ya tanuri kwa kutumia nishati ya kuni hasa katika maeneo ya mijini na badala yake imewataka waTU watumie pumba kama nishati mbadala ya kuchoma matofali hayo.

Onyo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu wakati alipokuwa akizungumza na kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Geita ikiwa ni ziara yake ya kwanza ya kikazi kwa mikoa ya Kaskazini Magharibi tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo.

Amesema uchomaji matofali kwa kutumia nishati ya kuni umekuwa ukichangia  upotevu mkubwa  wa misitu hali inayotishia sehemu kubwa ya nchi kuwa na jangwa.

Amesisitiza kuwa  matofali yachomwe kwa kutumia pumba za mazao badala ya kuni hali itakayopelekea kunusuru nchi kuwa jangwa huku akiagiza kamati hiyo ya mkoa huo kuanza kulisimamia agizo hilo mara moja.

Amesema katika sehemu kubwa ya nchi kwa sasa, uharibifu wa mazingira  umeongezeka kufuatia ukataji miti ovyo kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kibinadamu ikiwemo  uchomaji wa matofali kwa kutumia kuni.

"Mimi sipo tayari kuona nchi inageuka kuwa  jangwa lazima nisimamie kwa kuanza  katika maeneo ya mjini kama vile Geita unakutana na  tanuri za kuchoma matofali kwa kutumia kuni, hili sikubaliani nalo," amesisitiza Mhe.Kanyasu.

Amesema kwa mujibu wa takwimu, Tanzania imekuwa ikipoteza zaidi ya hekta 372,000 za misitu nchini kila mwaka.