Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, samwel Sitta
Maandalizi ya mkutano wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki unaotarajiwa kufanyika jijini Arusha siku ya Tarehe 30/04/2014 yamekamilika ambapo marais wa nchi zote Tano wanatarajiwa kupokea mapendekezo mbalimbali ya baraza la mawaziri wa nchi hizo.
Waziri wa ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania Mh Samweli Sitta ametaja baadhi ya mapendekezo yatakayowasilishwa kwenye kikao hicho kuwa ni pamoja na hatua iliyofikiwa katika michakato mbalimbali inayoaendelea ukiwemo wa uundwaji wa shirikisho la kisiasa.
Mh Sitta ameongeza pia kuwa mapendekezo juu ya maombi ya nchi ya Sudani Kusini kujiunga kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki yatawasilishwa.
Awali akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa maktaba ya Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyozinduliwa na mwenyekiti wa baraza la mawaziri wa Jumuiya hiyo Bi Phillis Kandie, Mh Sitta amesema baada ya kupatikana kwa maktaba ya Jumuiya, nyaraka na kumbukumbu zilizoko katika maeneo mbalimbali ya nchi wanachama zinatarajiwa kurejeshwa kwenye maktaba hiyo
Naye mwenyekiti wa baraza hilo Bi. Phills Kandie amesema kupatikana kwa maktaba hiyo ni hatua kubwa kwa Jumuiya na ina umuhimu mkubwa na itasaidia kurahisisha utekelezaji wa masuala mbalimbali ya maendeleo ya nchi wanachama Jumuiya