Friday , 5th Jul , 2019

Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, amehakikisha kuwa, Tanzania na Kenya zitaendelea kuwa nchi zenye kudumisha undugu, na kamwe kutoruhusu maneno yoyote yenye kuleta ulaghai na mgawanyiko.

Rais Magufuli

Rais Magufuli ameyabainisha hayo leo Julai 5, katika uwanja wa ndege wa Chato mkoani Geita, mara baada ya kumpokea mgeni wake Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, aliyekuja hapa nchini kwa ziara yake binafsi.

''Sisi ni ndugu na siku zote tutatembea pamoja, sisi ni ndugu na tusikubali kulaghaiwa na tukadhani kuwa wakenya na watanzania ni watu tofauti''.

Aidha Rais Magufuli amemshukuru Rais kenyatta, kwa kuendelea kuudhihirisha umma na dunia nzima kwamba, Tanzania na Kenya ni marafiki wa kufa na kupona, na utadumu katika maisha yote.

''Nikupongeze Mheshimiwa Rais Kenyatta pamoja na Serikali ya Kenya kwa ujumla, kwa hatua mliyochukua kufuatia kauli iliyotolewa na mtu mmoja, akiwa na lengo la kuwagawanya watanzania na wakenya, umefanya vizuri sana, maneno yanayotoka kwenye ulimi wa binadamu huwa ni sumu kali.

Kwa upande wake Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amesema kuwa hakutegemea kama angekutana na umati wa watu namna ile, na yeye kama Rais wa nchi jirani na ndugu na Tanzania na rafiki wa Rais Dkt John Magufuli.

''Sisi kama viongozi kuhakikisha tunaondoa vikwazo vya ndugu zetu kutembeleana, kufanya biashara, kuoana na hii ndio njia ya kumaliza ukabila, na mambo mengine yanayotugawanya''

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, ndio Rais wa kwanza kutoka nje ya nchi, kufika Wilaya ya Chato katika Mkoa wa Geita na atakuwepo nchini kwa siku mbili.