Mwenyekiti mwenza wa Umoja ya Katiba ya Wananchi (UKAWA) James Mbatia ameliomba bunge kuahirisha shughuli zake za kawaida,ili kujadili tukio la wizi na usambazaji wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali inayohusu uchunguzi wa wizi wa shilingi bilioni 321 fedha zilizokuwa katika ya akaunti ya Tegeta ya Escrow.
Hoja hiyo ya Mheshimiwa Mbatia ambaye ni Mbunge wa Kuteuliwa imefuatia taarifa kuwa ripoti hiyo imesambaa mitaani mjini Dodoma huku kurasa zikiwa zimenyofolewa ili kupoteza ushahidi.
Mheshimiwa Mbatia amesema inavyoonekana taarifa hiyo imeibwa na kusambazwa baada ya kupokelewa na Ofisi ya Katibu wa Bunge kinyume cha kifungu namba 31 kifungu kidogo cha Tisa ( G) cha Sheria ya haki, kinga na madaraka ya Bunge ambacho kimeainisha ni kosa kwa mtu yeyote kusambaza nyaraka iliyoandaliwa kuwasilishwa bungeni kabla ya wakati wake.
Akijibu hoja hiyo, Spika wa Bunge Mheshimiwa ANNA MAKINDA amesema ofisi yake kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi imezuia kumwachia mtuhumiwa wa usambazaji wa taarifa hiyo, ili aweze kusema mahali alipoitoa taarifa hiyo pamoja na vifaa alivyotumia ,ili viweze kukamatwa.
Hata hivyo maelezo hayo ya spika hayakukubaliwa na idadi kubwa ya wabunge wa UKAWA ambao wameomba mwongozo wa spika kwa maelezo kuwa mjadala huo unalenga kujadili haki, kinga na madaraka ya bunge, baada ya baadhi ya wabunge kupitishiwa nyaraka za kuchafuliwa, chini ya milango wakwemo wajumbe wa kati ya PAC.
Waziri kivuli wa wizara ya nishati na madini ambaye pia ni miongoni mwa viongozi wa UKAWA Mheshimiwa John Mnyika amedai mtuhumiwa huyo ana uhusiano na mmoja na viongozi wa wizara hiyo, hivyo amemtahadharisha spika kuwa iwapo mtuhumiwa huyo atapelekwa mahakamani, badala ya kujadiliwa bungeni ofisi ya spika itaonekana kuhusika.