Wednesday , 7th Sep , 2016

Soko la Hisa la Dar es Salaam limeyataka makampuni kujitokeza kwa ajili ya kupatiwa huduma ya ushauri wa kitaalamu wa jinsi makampuni hayo yanavyoweza kujisajili na kuuza hisa zao katika soko hilo.

Meneja Miradi na Biashara wa DSE Bw. Patrick Mususa (aliyesimama) akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam hivi karibuni

Meneja Miradi na Biashara wa Soko hilo Bw. Patrick Mususa amesema hayo katika mahojiano na EATV jijini Dar es Salaam leo na kwamba soko la hisa lina fursa nyingi zinazoweza kuyainua makampuni hususani yale yanayotafuta mitaji kwa njia ya kuuza hisa na hati fungani.

Kauli ya Mususa imekuja wakati ambapo ukubwa wa mtaji wa soko ukiwa umeshuka kwa asilimia 8.5 kutoka mtaji wenye thamani ya shilingi za Tanzania trilioni 22.8 hadi shilingi trilioni 20.9 kwa mujibu wa taarifa za mwenendo wa biashara katika soko hilo kwa kipindi cha wiki moja iliyopita.

“Katika kipindi hicho, ukubwa wa mtaji wa makampuni ya ndani pia umeshuka kwa asilimia 1.6 kutoka shilingi trilioni 8.3 hadi Trilioni 8.2 huku idadi ya mauzo ikiwa imeongezeka kwa asilimia 73 na kufikia shilingi bilioni 3.8 kutoka mauzo yenye thamani ya shilingi bilioni 2.2 juma moja lililopita,” amesema Mususa.

Aidha amesema viashiria vya soko vinaonesha kuwa sekta ya viwanda wiki hii imeshuka kwa pointi 95.63 tatizo ambalo pia limeigusa sekta ya huduma za kibenki na kifedha, huku sekta ya huduma za kibiashara ikiwa iimebakia kwenye kiwango kile kile kilichokwepo wiki iliyopita.