Waziri Mkuu akizungumza na wananchi wilayani Karatu
Ametoa ushauri huo wakati akifungua tawi la benki ya Biashara ya Uchumi lililopo wilayani Karatu mkoani Arusha akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani hapa.
Alisema tabia ya baadhi ya wananchi kuhifadhi kiasi kikubwa cha fedha majumbani si nzuri kwa sababu wanahatarisha usalama wao, hivyo ni vyema wakatumia benki mbalimbali zilizoko kwenye maeneo yao kwa ajili ya kutunza fedha zao.
Akizungumzia kuhusu kufunguliwa kwa tawi la benki ya Uchumi wilayani Karatu, Waziri Mkuu alisema unaashiria ukuaji wa uchumi wa wilaya hiyo kwa kuwa benki ni kichocheo cha maendeleo.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu aliushauri uongozi wa benki ya Uchumi kuangalia uwezekano wa kupunguza kiasi cha riba wanachokitoza katika mikopo wanayoitoa ili kuwawezesha wananchi kukopa na kupata tija.

Benki ya Uchumi ilianzishwa Septemba 22, 2005 ikiwa na mtaji wa sh. milioni 372. Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Oktoba, 2016 mtaji huo umefikia sh. bilioni 5.4 hivyo umeongezeka mara 14.5 zaidi ya ule wa awali uliokuwepo wakati wa uanzishwaji wake.



