Wednesday , 30th Nov , 2016

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameongoza mamia ya waombolezaji kuaga mwili wa marehemu Mzee Xavery Pinda ambaye ni baba mzazi wa Waziri Mkuu Mstaafu Mheshimiwa Mizengo Pinda.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akitoa heshima za mwisho kwa marehemu Xavery Pinda

 

Akizungumza wakati wa kuaga mwili huo nyumbani kwa Mheshimiwa Pinda kijijini Zuzu, Manispaa ya Dodoma  leo  Waziri Mkuu ametoa pole kwa wanafamilia na kuwaomba waendelee kumuombea marehemu apumzike mahala pema peponi.

Mzee Xavery alifariki dunia Novemba 27, 2016 saa 9.30 alasiri katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma alikokuwa amelazwa akipatiwa matibabu.

Amesema msiba huo ni mzito, hivyo anawaomba wanafamilia wawe watulivu na moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mpendwa wao.

Wakati huo huo Waziri Mkuu amemuhakikishia Mheshimiwa Pinda kwamba Serikali iko pamoja naye katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mzazi wake.

Naye Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dk. Jakaya Kikwete amesema marehemu Mzee Xavery alikuwa mwema sana na alikuwa na upendo kwa watu wote.

“Baba yake Pinda alikuwa baba yangu pia. Alitambua ugumu wa kazi tulizokuwa tunazifanya na alitutaka tuwe wavumilivu,” amesema.

Kwa upande wake Mheshimiwa Pinda aliwashukuru viongozi wa Serikali, vyama vya siasa na wananchi kwa kutenga muda wao na kwenda kumfariji kufuatia msiba huo mzito. “Kuondokewa na baba mzazi au mwanafamilia yeyote si jambo dogo”.

Awali akisoma wasifu wa marehemu, Edward Kyungu ambaye ni mjukuu alisema Mzee Xavery alizaliwa mwaka 1926 katika kitongoji cha Mbede akiwa ni mtoto wa pekee wa Mzee Mizengo Pinda na Mama yake Wakalyate (Umartina).

Askofu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani Dkt. Alex Malasusa akimpa pole Mizengo Pinda

 

Mzee Xavery alikuwa Katekista kazi ambayo aliifanya kuanzia mwaka 1951 hadi 1972 alipoamua kustaafu.

“Kazi ya pili ambayo alianza kuifanya kabla na hata wakati wa Ukatekista ni ukulima, jambo ambalo amewarithisha  watoto wake wote na ndio maana wameachiwa sifa moja ya kuitwa watoto wa mkulima,” amesema.

Mzee Xavery anatarajiwa kuzikwa kesho (Alhamisi, Desemba Mosi, 2016) katika kijiji cha Kibaoni wilaya ya Mlele mkoani Katavi. Marehemu ameacha mke, watoto wanane, wajukuu 54 na vitukuu 40.