Tuesday , 23rd Dec , 2014

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam nchini Tanzania leo itaanza kusikiliza kesi ya maombi ya makampuni ya kuzalisha umeme ya IPTL na PAP ya kutaka kuzuia utekelezaji wa maazimio ya Bunge kuhusu kashfa ya akaunti ya Tegeta Escrow.

Jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Kesi hiyo jana ilipangiwa majaji watatu ambao ni Jaji kiongozi Augustine Mwarija, Jaji Gadi Mjemas pamoja na Jaji Stela Mugasha.

Kwa mujibu wa hati ya kesi hiyo, IPTL na PAP inadai kwamba kilichofanyika ndani ya Bunge ni kinyume cha Katiba ya Jamhuri na kina lengo la kugombanisha mihimili mitatu ya dola yaani Bunge, Mahakama na Serikali.

Hati hiyo inadai kwamba maazimio ya Bunge yanakiuka Ibara ya 13(1) ya Katiba ya Tanzania inayosema watu wote ni sawa mbele ya sheria na wanastahili kutendewa haki bila kubaguliwa.

Hata hivyo Maazimio hayo ya Bunge yameshaanza kutekelezwa na Rais wa Jahmuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwawajibisha wahusika ambapo jana Rais Kikwete alitengua uteuzi wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Mandeleo ya Makazi Prof Anna Tibaijuka huku Waziri wa Nishati na Madini akiwekwa Kiporo.