Tuesday , 25th Nov , 2014

Jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam chini ya Jaji Radhia Sheikhe limezuia mjadala wa ripoti ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa serikali kuhusu akaunti ya Tegeta Escrow.

Jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam chini ya Jaji Radhia Sheikhe limezuia mjadala wa ripoti ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa serikali kuhusu akaunti ya Tegeta Escrow hadi hapo hoja ya msingi ambayo ipo mahakamani itakapofanyiwa kazi.

Jopo hilo lililokuwa likiongozwa na Mh Radhia Sheikhe wameagiza kutofanyika kwa mjadala wotote kuhusu Ripoti ya CAG huko Bungeni na kuongeza kuwa majadiliano hayo yanaweza kufanyika baada ya shauri la msingi kupatiwa ufumbuzi.

Awali mwanasheria wa IPTLl wakili Joseph Makandege amesema wamefikisha shauri hilo namba 50 katika mahakama hiyo wakitaka vifanyike vitu viwili kwanza kupata tafsiri sahihi ya kisheria kuwa kama kitendo kilichofanywa na ofisi ya CAG kufanya ukaguzi katika akaunt za Escrow kama ni sahihi akaongeza kuwa wao wanachoamini ni kuwa kwa sababu jambo hilo lilikuwa limekwisha amuliwa kisheria na mahakama na kwa kutolewa kwa hukumu kulikuwa hakuna haja tena na bunge kuagiza uchunguzi ufanyike.

Aidha mwanasheria huyo akaongeza kuwa siyo kwamba hawataki jambo hilo kujadiliwa bali wanataka taratibu zifuatwe ili kuweza kufikia mwafaka wa kina katika jambo hilo.

Mwanaasheria huyo akaongeza kuwa mbali na kupata tafsiri hiyo ya kisheria pia wanaiomba mahakama kulitaka bunge kusitisha mpango wake wa kujadili tarifa ya CAG hadi tafsiri ya kina ipatikane.

Mwanasheria huyo pia akasema kuwa wao wanaona kama likijadiliwa haki haitaweza kutendeka kwa sababu wao kama IPTL hawana mwakilishi bungeni na hivyo maamuzi yatafanyika upande mmoja.

Kwa upande wa jopo la wanasheria wa serikali wakiongozwa na Obadia Kaimela wameiomba Mahakama kuwapa muda wa kuweza kuwasiliana na baadhi ya watu ama taasisi zinazohusishwa na jambo hilo ili kuweza kupata muda wa kutosha kutoa utetezi wao.

Kutokana na hali hiyo imeamuliwa kuwa baada ya kukamilika kwa taribu zote kesi ya msingi ikiwemo uwasilishwaji wa viapo kesi ya msingi itanza kusikilizwa Desemba 2 mwaka huu.

Hata hivyo Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali ameendelea kusisitiza kuwa kesho (26/11/2014) atatoa Ripoti Bungeni kuhusu upotevu wa pesa za ESCROW.

Zitto ametoa taarifa ifuatayo akinukuu Ibara ya 100 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977.

“Madaraka na Haki za Bunge
100.-(1) Kutakuwa na Uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu katika Bunge na Uhuru huo hautavunjwa wala kuhojiwa na chombo chochote katika Jamhuri ya Muungano, au katika Mahakama au mahali penginepo nje ya Bunge
Kesho tarehe 26 Novemba 2014 Bunge litajadii Taarifa ya PAC kuhusu uchotwaji wa Fedha kutoka akaunti ya #TegetaEscrow “

Kwa mujibu wa mwanasheria Lilian Elias akiwa katika kipindi cha #HOTMIX EATV, amesema kuwa, Kwa kuwa bado mjadala wa Escrow haujafanyika na Bunge halijafanya maamuzi yoyote kuhusu hilo kiasi cha kumuthiri mtu yoyote, MAHAKAMA HAINA NGUVU KIKATIBA NA KISHERIA KUZUIA MJADALA HUO.