Wednesday , 23rd Mar , 2016

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi amepiga marufuku shirika la Nyumba nchini, (NHC),kuanzisha miradi mingine ya Ujenzi pamoja na kupandisha kodi bila kumtaarifu.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Nehemia Mchechu

Akizungumza katika Mkutano wake na Bodi pamoja na Menejimenti ya Shirika la Nyumba, jana Jijini Dar es Salaam Mhe. Lukuvi ameagiza shirika hilo limalizie miradi yake zaidi ya saba ambayo inaendelea hivi sasa.

Waziri Lukuvu ameitaka bodi na Menejiment ya shirika hilo kusimamia miradi hiyo kukamilika kwa wakati ikiwa ni pamoja na kuondoa changamoto zilizopo ambazo zinawachelewesha katika umaliziaji wa miradi hiyo.

Aidha Waziri Lukuvi amepiga marufuku upandishwaji wa kodi za nyumba za NHC bila kibali kutoka kwake ingawa shirika hilo lina mamlaka ya kujipangia kiwango cha kodi wanayoitaka.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodo ya shirika hilo Bi. Zakhia Meghji amesema bodi itatekeleza maagizo ya waziri, huku Mkurugenzi mtendaji wa Shirika hilo Nehemia Mchechu amesema baadhi ya changamoto alizozitaja waziri ameshaanza kuzishughulikia.