Monday , 31st Aug , 2015

Mgombea urais wa vyama vinavyounda (UKAWA) Mh. Edward Lowassa akiambatana na waziri mkuu mstaafu Mh. Fredrick Sumaye wameanza kazi ya kunadi sera zao mikoani katika mkoa wa Iringa huku wakiendelea kuungwa mkono na maelfu.

Wagombea Urais wa UKAWA Edward Lowassa na Juma Duni Haji.

Akizungumza na wananchi wa maeneo hayo mgombea urais huyo ameendelea kunadi sera za UKAWA na kuelezea azma yake ya dhati ya kufanya marekebisho makubwa na kwa wakati na kuzisimamia kikamilifu.

Katika hatua nyingine Shinikizo kutoka kwa wananchi limepelekea mgombea mwenza wa nafasi ya Urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Juma Duni Haji, kulazimika kumtangaza Maftaha Nachuma wa Chama cha Wananchi (CUF), kuwa mgombea ubunge katika jimbo la Mtwara mjini kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Maamuzi hayo yalitokana na wananchi waliojitokeza katika mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanywa na UKAWA leo katika viwanja vya mashujaa mkoani humo, kuwa na shauku ya kutaka kumjua mgombea wao.

Kwa upande wake, katibu wa kamati ya sheria na haki za binadamu wa CHADEMA kanda ya kusini, Hassani Mbagile, amesema wameyapokea maamuzi hayo kama yalivyoamuliwa na mgombea huyo lakini hayataishia hapo kwani watawasiliana na viongozi wa UKAWA ili kuhoji kama kuna uhalali wa mgombea kutoa maamuzi kutokana na shinikizo kutoka kwa wananchi.

Kwa upande wake, mgombea wa NCCR Uledi Hassan, alipotafutwa na East Africa Radio kuzungumzia maamuzi hayo alisema hawezi kuzungumza chochote kutokana na kuwa katika kikao.