Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu nchini Tanzania (LHRC) Dkt Hellen Kijo-Bisimba.
Akizungumza katika mahojiano na East Afrika Radio ofisini kwake jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mkuu wa kituo hicho Dkt. Hellen Kijo-Bisimba, amesema kituo hicho hakioni mantiki ya kuharakishwa kwa kura ya maoni, kwani hadi kufikia Machi mwakani tume ya taifa ya uchaguzi NEC itakuwa haijakamilisha uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.
Kauli ya Dkt Kijo-Bisimba inafuatia kauli ya mwanasheria mkuu wa serikali Jaji Frederick Werema kuwa serikali inakamilisha taratibu za maandalizi ya kura hiyo kufanyika mwezi Machi mwakani.
Kwa mujibu wa Dkt Bisimba ni kipindi kifupi kutoka sasa hadi mwakani na kwamba idadi kubwa ya Watanzania hawajaandaliwa kushiriki zoezi hilo na kwamba iwapo litafanywa kwa kulazimisha kama ambavyo serikali inafanya sasa, kuna kila dalili kuwa katiha itakayopatikana haitakuwa bora kwani itakuwa imekosa ridhaa ya umma mkubwa wa Watanzania.
Aidha, Dkt Bisimba amesema harakati za kutaka kuharakishwa kwa kura ya maoni zilionekana mapema tangu siku Bunge Maalumu la Katiba lilipopitisha katiba inayopendekezwa, na kwamba ni vema serikali ikasitisha mchakato wa kutafuta katiba mpya hadi baada ya uchaguzi mkuu wa Rais na wabunge mwakani kama ilivyopendekezwa hivi karibuni katika mkutano wa kituo cha demokrasia TCD na kukubaliwa na vyama vyote vyenye uwakilishi bungeni.