Tuesday , 28th Jun , 2016

Waziri Mkuu wa Lesotho, Dk. Pakalitha Mosisili amekubali kutekeleza masharti yaliyowekwa na Wakuu wa Nchi na Kamati ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika, SADC.

Bendera za nchi wanachama wa SADC.

Dk. Mosisili ametoa uamuzi huo leo wakati wa kikao maalum cha SADC na wakuu wa nchi wanaounda Kamati ya Siasa, Ulinzi na Usalama kilichofanyika jijini Gaborone, Botswana.
 
Pia amekubali viongozi wa upinzani na baadhi ya maofisa wa kijeshi wanaoishi uhamishoni ambao walikimbia machafuko yaliyotokea nchini humo warejee nchini mwao na kuahidi atahakikisha wanapatiwa ulinzi wa kutosha.
 
Kwa upande wake, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye alimwakilisha Rais Dk. John Magufuli katika kikao hicho amesema wamepitia ripoti iliyoundwa na timu ya SADC iliyochunguza kuhusu matatizo ya Lethoto ambayo iliwahoji Viongozi wa Serikali, Jeshi, Bunge na familia ya marehemu Luteni Jenerali Mahao.
 
Mh. Majaliwa amesema, lengo la hatua hizo za SADC ni kuhakikisha inarejesha hali ya amani na utulivu kwenye maeneo ya siasa, ulinzi na usalama katika nchi wanachama wa Jumuiya hiyo ili wananchi wake waweze kuishi vizuri,
 
Pia Waziri Mkuu amesema Tanzania inatarajiwa kukabidhiwa uenyekiti wa Wakuu wa Nchina Serikali na Kamati ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Uchumi na Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC Double Troika Summit), Agosti mwaka huu ambapo kitafanyika kikao kingine nchini  Tanzania.
 
Mkutano huo wa ulifunguliwa na Rais wa Botswana, Mhe. Lt. Jen. Seretse Khama Ian Khama na ulihudhuriwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye alikuwa akimwakilisha Rais Dk. John Pombe Magufuli;  Rais wa Afrika Kusini, Bw. Jacob Zuma; Rais wa Msumbiji, Bw. Filipe Jacinto Nyusi; Rais wa Zimbabwe, Bw. Robert Mugabe, Mfalme Muswati wa III wa Swazland.