Wednesday , 10th May , 2017

Waziri kivuli wa Mambo ya Ndani, Mh. Godbless Lema amefafanua kuwa majeshi la polisi pamoja na magereza yanashindwa kufanya kazi kwa ufanisi kutokana na fedha finyu wanazopatiwa na serikali ikiwa ni pamoja na kutoboreshwa kwa maslahi yao.

Akizungumza Bungeni wakati anawasilisha hotuba ya kambi ya upinzani , Mh Godbless Lema amesema ni mara nyingi majeshi hayo yamekuwa yakitupia lawama serikali kwa kushindwa kuwapatia stahiki zao mapema zikiwepo posho na mishahara jambo ambalo linawapelekea kufanya kazi bila morali.

"Askari wasiokuwa na maslahi mazuri na bora ni hatari sana kwa taifa, msicheze na maslahi ya askari wetu, naiomba serikali ianze kuwalipa mishahara mizuri pamoja na posho kama jinsi inavyofanya kwa watumishi wengine wa umma ikiwa ni pamoja na wabunge na mawaziri - Lema alifunguka."

Pamoja na hayo Lema ambaye ni Mbunge wa jimbo la Arusha mjini (CHADEMA), ameongeza kwamba serikali imewasusa sana watumishi hao hali ambayo inawapelekea kufanya kazi katika mazingira magumu kuanzia kwenye suala la malazi, ofisi hadi vitendea kazi vyake.

"Mh. Mwenyekiti, ufinyu wa bajeti kama jinsi unavyosemekana umesababisha ukosefu wa nyumba za watumishi na maaskari, upungufu wa vyombo vya usafiri, watumishi, ofisi stahiki ya wakuu wa magereza, vifaa vya kufanyia kazi, hata nilipoenda magereza Kisongo ilibidi niwanunulie computer kwa ajili ya matumizi ya ofisi, mimi nilikuwa mahabusu mwema"- alisema Lema.