Mbunge wa Ulanga (CCM) Goodluck Mlinga
Mlinga ameyasema hayo katika kipindi cha East Afrika Breakfast Jijini Dar es salaam, Mlinga ameshiriki kama mtangazaji mwenza katika kipindi hicho ikiwa ni siku ya usiku wa Mapinduzi ambapo vipindi vyote vya redio vitakuwa na watangazaji wenza kutoka maeneo mbalimbali kulingana na aina ya kipindi.
''Suala la elimu bure halijawafurahisha wengi, maana walizoea kupiga hela kwa mtindo wa malipo ya vitu mbalimbali ambavyo wanafunzi hutakiwa kulipa'' Amesema Mlinga.
Mada ya elimu imetokana na mzazi mmoja ambaye mwanaye anasoma shule ya sekondari Kimange mkoani Pwani kueleza kwamba mwanae ametakiwa kurudi shuleni na shilingi laki mbili na tisini na mama huyo alipoenda shuleni, mkuu wa shule akamwambia uhamisho upo wazi kama huna fedha hizo.
Kufuatia hali hiyo Mbunge huyo amemchangia mzazi huyo shilingi laki moja na ishirini ili kusaidia mchango wa mwanafunzi huyo.
Aidha kwa upande wa serikali, Waziri wa TAMISEMI George Simbachawene amesema walimu hawatakiwi kuwafukuza wanafunzi bali wanatakiwa wakae na wazazi kuangalia gharama zinazotakiwa za ulazima na wakubaliane namna ya malipo, ila wanafunzi wasifukuzwe kwenda kutafuta madeni.





