Sunday , 7th May , 2017

Rais Magufuli ameamuru taasisi zinazofanya kazi na Mamlaka ya Bandari(TPA), zikiwamo Shirika la Viwango(TBS), Mamlaka ya Chakula(TFDA), Mamlaka ya Mapato (TRA) na kampuni za uwakala wa forodha, kufanya kazi saa 24 ili kuondoa ucheleweshaji wa mizigo.

Rais Magufuli, ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Biashara, akiongoza mkutano wa baraza hilo Ikulu jijini Dar es salaam jana. Wengine ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (kushoto) na Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Dk. Reginald Mengi.

Magufuli alitoa agizo hilo jana Ikulu jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza kwenye mkutano wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC).  Alisema kuanzia kesho (leo)  taasisi hizo zifanye kazi kwa saa 24.

Alisema haiwezekani Bandari ya Dar es Salaam itumie siku 14 kutoa mzigo wakati Mombasa inatumia siku tatu hadi nne tu.

Magufuli alifikia uamuzi huo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania Tatoa), Angelina Ngakula, kwamba taasisi hizo zimekuwa zikichangia katika ucheleweshaji wa mzigo na kujikuta wanatumia hadi wiki mbili kupakia mizigo yao. 

Alisema wamejikuta wanapoteza muda mwingi kwenye Bandari ya Dar es Salaam kutokana na kukosekana kwa ushindani hivyo kupoteza soko la tani milion tatu katika nchi nyingine kutokana na ucheleweshaji huo.

Aidha, Angelina alisema kukosekana kwa tani hizo kunaikosesha serikali Sh. trilion moja kutokana na wateja kuogopa kutumia bandari hiyo kwa kuhofia ucheleweshaji.

"TPA (Mamlaka ya Bandari) wameboresha (huduma zao) ila hizo taasisi nyingine hawafanyikazi kwa saa 24," alisema Angelina. "Yaani hakuna mawasiliano baina ya hizo taasisi."

"Tunapata shida katika kutoa mizigo na haileti ushindani katika bandari nyingine maana kule Mombasa mzigo unaupata ndani ya siku tatu ama nne."