Wednesday , 29th Oct , 2014

Ofisi ya Taifa ya Takwimu nchini imetoa chapisho kuu la utafiti wa mapato na matumizi ya kaya binafsi linaloonesha kuwa kiwango cha umasikini hasa wa mahitaji muhimu ya kaya kimepungua kutoka asilimia 34 mwaka 2007 hadi asilimia 28 mwaka 2011.

Waziri wa Fedha na Uchumi nchini Tanzania, Bi. Saada Mkuya Salum.

Akizungumza katika uzinduzi wa chapisho hilo, Waziri wa Fedha na Uchumi nchini Mhe. Saada Mkuya Salum amesema utafiti huo umebaini kuwa hata idadi ya Watanzania wanaopata huduma za afya katika hospitali za umma imeongezeka kutoka asilimia 41.6 hadi asilimia 55.

Hata hivyo Waziri Mkuya amesema kasi ya kupunguza umasikini imekuwa ni ndogo hasa kutokana na idadi kubwa ya watanzania kutegemea sekta za kilimo na uvuvi huku kiwango cha matumizi ya zana za kisasa katika sekta hizo yakiwa ya chini.

Awali, Murugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt Albina Chuwa amesema utafiti huo unatoa picha pana ya hali ya maisha ya Watazania pamoja na mafanikio ya mipango mbalimbali ya kupunguza umasikini ambayo serikali inaitekeleza hivi sasa.

Dkt Chuwa amesema inatia faraja kuona kuwa idadi kubwa ya watanzania wanaishi kwenye mstari wa umaskini ambao ni kuwa na pato la zaidi ya shilingi elfu Thelathini kwa mwezi, pato ambalo linahitaji juhudi ndogo tu kuweza kulivusha kundi hilo na kuwa nchi yenye watu wa kipato cha wastani.

Kwa upande wake, Gavana wa benki Kuu Profesa Beno Ndulu amesema kiwango cha watu wanaopata huduma za kibenki katika kipindi hicho nayo imeongezeka na kufikia asilimia 55 ya watu wazima wenye uwezo wa kutumia huduma za kibenki.

Hata hivyo, Gavana Ndulu amesema bado benki za biashara nchini hazijawa rafiki kwa wakulima na kwamba tegemeo pekee la serikali hivi sasa ni upatikanaji wa huduma za kibenki kwa kupitia teknolojia za kisasa mfano huduma zinazotolewa kupitia simu za mkononi.

Profesa Ndulu amesema teknolojia ya kutuma na kupokea pesa kwa njia ya simu za mkononi imepunguza usumbufu wa kutuma na kupokea pesa kwa watu wanaoishi maeneo ya vijijini na kwamba serikali inaendelea kuhimiza wananchi kujiunga na vikundi vidogo vidogo vinavyotoa mikopo ya pesa, mahali ambako amesema ndio wanakoweza kupata mikopo yenye gharama nafuu kwao.