Thursday , 10th Jul , 2014

Rais Jakaya Kikwete amesema serikali imetenga shilingi milioni 500 kwa kila halmashauri ya wilaya nchini kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu ili kuwapunguzia adha na usumbufu walimu wanapopangiwa kwenda katika vituo vya kazi na kukosa makazi.

Rais wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.

Rais Kikwete ametoa ahadi hiyo wakati akizungumza na viongozi wa serikali, chama na wananchi wa tarafa ya Kimbe iliyopo wilayani Kilindi wakati akifungua maabara zinazojengwa chini ya sera ya kutaka kila shule ya sekondari iwe na maabara ili kuwanufaisha wanafunzi waweze kusoma masomo ya sayansi kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.

Kuhusu ujenzi wa shule za kata ambao amedai kuwa awali zoezi hilo lilipuuzwa na na kuitwa shule za yebo yebo, Rais Kikwete amesema ni shule zinazowaunganisha Watanzania tofauti na awali wanafunzi kufaulu ilikuwa ni kwa baadhi ya shule na ndio maana serikali imeanza kujenga shule hizo kisha kusomesha idadi kubwa ya walimu ikifiatiwa na maabara ili kuweka uwiano wa kielimu nchini.

Awali akielezea changamoto wanazokabiliana nazo, wakazi wa tarafa ya Kimbe wilayani Kilindi, mbunge wa jimbo hilo Bi. Beatrice Shelukindo amesema wakazi wa eneno hilo wanalazimika kuuza debe moja la mahindi kwa shilingi 2,400 hivyo amemuomba Rais Kikwete kuwashawishi hifadhi ya taifa ya chakula ya chakula kununua mazao yao ili kunusuru nguvu za wakulima zisipotee bure.