Tuesday , 8th Dec , 2015

Rais Mstaafu wa Tanzania wa awamu ya nne Dr. Jakaya Mrisho Kikwete kesho Tar 09/12/2015 ataadhimisha siku ya uhuru wa Tanganyika kwa kushiriki katika kufanya usafi katika hospitali ya Chalinze katika mkoa wa pwani.

Rais Kikwete atasheherekea sikukuu hii kwa staili ya tofauti kabisa ukilinganisha na ilivyozoeleka kwa miaka 53 mfululizo, kwa kujumuika katika uwanja wa Taifa na kushiriki maonyesho mbalimbali ya kijeshi na kitamaduni na kuhudhuriwa na viongozi kutoka ndani na nje ya nchi na maelfu ya wananchi.

Pamoja na umuhimu mkubwa uliopo kwa kumbukumbu hii muhimu kwa nchi yetu, mwaka huu katika serikali hii ya awamu ya tano ikiongozwa na Rais Dr. John Magufuli inasherehekewa kwa aina yake ya kufanya usafi wa mazingira nchi nzima.

Dr. Magufuli alifikia uamuzi huu mgumu baada ya kasi ya ongezeko la ugonjwa wa kipindupindu kutapakaa katika mikoa mingi nchini, ikiongozwa na majiji ya Dar es salaam, Mwanza na Tanga na kusababisha vifo vya mamia ya wananchi.

Pamoja na hayo Rais Mh. Dr Magufuli alienda mbali zaidi na kutaka fedha kiasi cha shilingi bilioni 4 ambazo zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya sherehe ya siku hiyo ya uhuru zitumike katika ujenzi wa barabara kutoka Mwenge hadi Morocco jijini Dar es salaam, ili kuwezesha kupunguza kero ya foleni katika eneo hilo.