Dkt Charles Msonde - Katibu Mtendaji NECTA
Idadi hiyo ni sawa na ongezeko la wanafunzi 38,451 ikilinganishwa na wanafunzi 396,770 mwaka 2015.
Akiongea na waandishi wa habari hii leo kuhusiana na kuanza kwa mitihani hiyo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania Dkt. Charles Msonde amesema mitihani hiyo imeanza leo na itamalizika tarehe 25 Nov 2016.
"Wanafunzi 435,221 wamesajiliwa kufanya mitihani ya kidato cha pili 2016, wavulana ni 214,013 sawa na asilimia 49.17 na wasichana ni 221,208 sawa na asilimia 50.83. Watahiniwa wasioona ni 67 na watahiniwa wenye uono hafifu ni 306 ambao karatasi zao za mitihani hukuzwa," amesema Dkt. Msonde.
Wakati wanafunzi wa kidato cha pili wakiendelea na mitihani yao, Dkt Msonde amesema, wanafunzi wa darasa la pili katika shule za msingi zipatazo 17,032 kote nchi nao wanatarajiwa kufanya mitihani yao ya kuwapima uwezo tarehe 23 na 24 mwezi huu baraza hilo likiwakumbusha wasimamizi na wanafunzi kutojihusisha na udanganyifu wakati wa mitihani yao.
Aidha, Dkt. Charles Msonde amesema bado mitihani ya kidato cha nne kitaifa inaendelea na kwamba hadi hivi sasa baraza hilo halijapokea taarifa za kuvuja ama kushindwa kufanyika mitihani hiyo kama ilivyokusudia ambapo jamii imeshauriwa kutoingia maeneo ya shule ili kuwawezesha wanafunzi kufanya mitihani yao kwa utulivu na amani.