Saturday , 1st Nov , 2014

Kaya 480 zilizopokonywa ardhi na TANAPA na kukosa chakula kwa miaka nane, zameitaka serikali kutekeleza ahadi ya kuwapa ardhi mbadala ya kilimo na makazi ili kuepukana na mgogoro kati yake na hifadhi hiyo.

Wananchi wa kaya zaidi ya 480 katika vijiji vitatu wilayani Babati mkoani Manyara waliopokonywa ekari 17,000 na hifadhi ya taifa ya Tarangire (TANAPA) kwa madai ya kuvamia hifadhi hiyo kinyemela katika eneo walilopewa na serikali kupitia Operesheni vijiji wameitaka serikali kutekeleza ahadi ya kuwapa ardhi mbadala ya kilimo na makazi ili kuepukana na mgogoro kati yake na hifadhi hiyo.

Wakimlalamikia Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na maendeleo ya makazi Bw George Simbachawene wameeleza kuchoshwa na ahadi zilizotolewa na viongozi wa CCM na serikali za kumaliza mgogoro huo uliodumu kwa takribani miaka minane zikiwemo za kuwashawishi kufuta shauri mahakamani na kuwaacha njia panda changamoto iliyosababisha kuendelea kukosa chakula na makazi, licha ya hifadhi hiyo kulipa fidia isiyokidhi kwa kaya 171.

Kwa upande wake Mh. Simbachawene amesema kutokana na hoja za wananchi hao kuwa na mashiko amesema serikali itatoa mgawo kwa kaya 171 kutoka eneo la shamba la shirika la maendeleo la hanang lililopo wilayani babati lakini kwa kuwa eneo hilo halitoshi kuna kila sababu wizara yake na wizara ya mali asili na utalii kukutana ili kuona eneo hilo la ekari 17,000 linatolewa kwa kaya zilizokosa mgawo.

Hata hivyo kaimu mkuu wa mkoa wa Manyara ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Babati Bw Khalidi Mandia ameiomba wizara hiyo kulichukulia suala la ugawaji kwa uzito na haraka kwani licha ya kaya hizo 171 kutakiwa kupewa eneo hilo la shamba hilo tayari kaya 52 zimevamia shamba hilo la shirika la maendeleo.

Bado wilaya ya Babati inakabiliwa na migogoro mitano ambayo pia wananchi wake wanasubiria serikali kutoa uamuzi,miongoni mwa migogoro hiyo ni ule wa bonde la kiru na ule wa vilima vitatu kati ya wafugaji na mwekezaji.