Tuesday , 12th Jul , 2016

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anaeshughulikia Utumishi na Utawala Bora Mhe. Angela Kairuki amewataka wakurugenzi walioteuliwa waende kusimamia zoezi la kuwabaini watumishi hewa pamoja watoro makazini.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Utumishi na Utawala Bora Mhe. Angellah Kairuki.

Akizungumza leo wakati wa Kiapo cha Maadili kwa Wakurugenzi wa Wilaya nchini, Jijini Dar es Salaam, Waziri Kairuki amesema kuwa tatizo la watumishi hewa wengi lipo kwenye serikali za mitaa ambapo asilimia 90, ya watumishi wote hivyo amewataka kufuatilia suala hilo kwa ukaribu zaidi.

Waziri Kairuki amesema mpaka sasa serikali imeshawabaini watumishi hewa 12246, hadi mwisho wa mwezi Mei na bado serikali inaendelea kuwaondoa watumishi hao hadi mwishoni mwa mwezi wa nane huku akisisitiza serikali imesimamisha zoezi la ajira serikali ili kupambana na sakata hilo.

Aidha Mhe. Kairuki amewataka wakurugenzi hao kusoma sheria mbalimbali ili waepuka muingiliano wa kimadaraka na viongozi wengine lakini pia waisome vizuri sheria mpya ya manunuzi ya umma ili kuepuka kuingia katika manunuzi yatakayoitia hasara serikali.

Amesema kuwa kutokana na suala hilo serikali itawachukulia hatua maafisa utumishi ambao walipewa dhamana la kusimamia watumishi hao ambapo wengi wao ndio wamekua chanzo cha uwepo wa watumishi hewa.