Tuesday , 9th Sep , 2014

Mkutano wa Rais Kikwete na Kituo cha Demokrasia umekubaliana kwamba Katiba mpya ipatikane baada ya uchaguzi mkuu wa 2015 lakini Bunge la Katiba liendelee na vikao vyake.

Rais Jakaya Kikwete akizungumza na Wajumbe wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TDC) wakati alipokutana nao kwenye Ikulu ndogo Dodoma

Viongozi wakuu wa vyama vya Siasa vyenye wabunge vinavyounda kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) na wale wa vyama visivyokuwa na wabunge wamekutana na Rais JAKAYA KIKWETE mjini Dodoma na kukubaliana kutumika kwa Katiba ya sasa iliyotungwa mwaka 1977 katika Uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015.

Makubaliano hayo yamefikiwa baada ya kufanya majadiliano ya kina na kubaini kuwa mchakato wa Katiba unaoendelea hivi sasa hauwezi kufikia mwisho kwa muda uliopangwa na hivyo kuamua kuendelea kwa Bunge la Katiba mpaka pale litakapotoa Katiba inayopendekezwa ambao ndiyo utakuwa mwisho wa mchakato huo kwa sasa.

Mwenyekiti wa TCD JOHN CHEYO akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma akiambatana na viongozi wa vyama vingine vya Siasa amesema iwapo mchakato huo utatakiwa kufikia mwisho ipo haja ya kusogeza mbele Uchaguzi mkuu ujao jambo ambalo limekataliwa hivyo mchakato wa kutunga Katiba utaendelea mwaka 2016 baada ya Uchaguzi Mkuu.

Mhe. Cheyo ameeleza kuwa kamati zote zilitoa taarifa zao kwenye vikao vya Viongozi Wakuu wa Vyama (Summit) ya TCD ambayo wajumbe wake ni Wenyeviti, Makamu Wenyeviti na Makatibu Wakuu wa Vyama wanachama.

< Mhe. Cheyo aliongeza kuwa katika kutafuta maridhiano, Wenyeviti na Makatibu Wakuu wa Vyama walifanya mashauriano na Mhe. Rais Dkt.
Jakaya Mrisho Kikwete siku ya tarehe 31 Agosti mwaka huu, hivyo tarehe Nane Septemba, 2014 hapa Dodoma wakatoa tamko lao

Pamoja na kazi ya msingi inayofanywa na Bunge Maalum la Katiba, mchakato wa Katiba unaoendelea sasa hauwezi kutupa Katiba itakayotumika katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa kuwa muda hautoshi kukamilisha mchakato na kufanya mabadiliko yatakayohitajika ya Sheria, Kanuni na Taasisi
mbalimbali zitakazohitajika”, alisema Mhe. Cheyo

Mhe. Cheyo aliendelea kwa kusema kuwa, kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba mwisho wa mchakato ni kura ya maoni itakayofanyika mwezi Aprili 2015

“Kama itabidi kura irudiwe kwa mujibu wa Sheria iliyotajwa, kura itarudiwa mwezi Juni au Julai 2015, muda ambao Bunge la Jamhuri ya Muungano linatakiwa livunjwe kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba 2015 na ili Katiba Mpya itumike katika uchaguzi Mkuu utakaokuja, itabidi uhai wa Bunge na Serikali uongezwe zaidi ya 2015, jambo ambalo hatuliungi mkono”, alisisitiza Mhe. Cheyo.

Akiongelea juu ya Tangazo la Serikali GN Na 254, Mhe. Cheyo amesema kuwa Bunge Maalum la Katiba kwa sasa linafanya kazi kwa mujibu wa
Tangazo la Serikali (Government Notice) Na 254 lililotolewa na Mhe. Rais Kikwete tarehe 1 Agosti, 2014

“Tangazo hilo litatumika hadi tarehe 4 Oktoba, 2014 ambapo Katiba inayopendekezwa inategemewa kupatikana, Wajumbe walikubaliana hatua hii iachwe ifikiwe”, alisema Mhe. Cheyo

Kuhusiana na Kura ya maoni, Mhe. Cheyo ameeleza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba baada ya Bunge hilo kumaliza kutunga Katiba, ingefuata hatua ya kura maoni kuthibitisha Katiba

“Kwa kutambua kuwa hatua ya kura ya maoni italazimisha uchaguzi mkuu 2015 kualishwa, basi hatua hii iailishwe, na mchakato wa Katiba uendelee baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015”, alisema Mhe. Cheyo

Sambamba na hayo, Mhe. Cheyo ameishauri Serikali kuchukua hatua za kisheria ili matayarisho kwa ajili ya Uchaguzi wa Vijiji, Vitongoji na Mitaa, yaanze haraka iwezekanavyo ili uchaguzi ufanyike mapema hapo mwakani

Aidha, amegusia kuhusu Mabadiliko ya 15 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 akasema kuwa, kwa vile Uchaguzi Mkuu wa
2015 utafanyika kwa kutumia Katiba ya 1977, kuna umuhimu kufanya mabadiliko kidogo (minimum reforms) katika Katiba pamoja na sheria ya Uchaguzi yatayowezesha nchi kufanya uchaguzi huru na wa haki

“Tayari mambo yafuatayo yamekubaliwa, kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi kusimamia uchaguzi, Mshindi wa Uchaguzi wa Rais ashinde kwa zaidi ya asilimia 50% (50%+1)”, alisema Mhe. Cheyo

Viongozi hao Wakuu wa Vyama wamempongeza Mhe. Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa ujasiri wake na imani yake katika kuimarishademokrasia nchini na kuanzisha mchakato wa kuandika Katiba Mpya ya nchi.

Aidha CHEYO amesema yapo marekebisho ambayo yameridhiwa kufanyika katika Katiba ya sasa ikiwemo kuweka suala la Mgombea binafsi na kutoa wito kwa vyama na wadau mbalimbali wenye marekebisho wanayotaka yawemo katika Katiba mpya kuyawasilisha mapema.

Kikao hicho kilichoketi Septemba Nane mwaka huu mjini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi kutoka CCM, CHADEMA, NCCR MAGEUZI, CUF na UPDP kilitarajiwa kutatua utata wa kurejea au kutorejea kwa Wajumbe wa Bunge la Katiba kutoka kundi la UKAWA waliosusia vikao hivyo ingawa Mwenyekiti wa TCD JOHN CHEYO amesema suala la UKAWA halikuwa ajenda kwenye kikao hicho