Kasi ya Mfumuko wa bei ya Taifa ya bidhaa kwa mwezi Desemba 2015 umeongezeka hadi asilimia 6.8 kutoka asilimia 6.6 tofauti na ilivyokuwa mwezi Novemba 2015.
Mkurugenzi wa sensa na Takwimu za jamii kutoka NBS Ephraim Kwesigabo amesema leo jijini Dar es salaam wakati akitoa taarifa ya mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwezi Desemba 2015 ambayo inaonesha kasi ya kupanda kwa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioisha mwezi December 2015 imeongezeka ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioisha mwezi November 2015.
Kwesigabo amesema fahirisi za bei zimeongezeka hadi 161.24 kwa mwezi Desemba 2015 kutoka 150.92 mwezi Desemba 2014.
Aidha mkurugenzi huyo amesema uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma umefika Shilingi 62 na senti 02 mwezi Desemba 2015 kutoka mwezi Septemba 2010 ikilinganishwa na shilingi 62 na senti 31 ilivyokuwa mwezi Novemba 2015 na mfumuko huo wa bei nchini una mwelekeo unaofanana na baadhi ya nchi nyingine za Afrika Mashariki.