Tuesday , 6th May , 2014

Kamati Kuu ya CCM imekutana leo mjini Dodoma kwa dharura na kujadili masuala kadhaa ikiwa ni pamoja na mwenendo wa mchakato wa kupata Katiba mpya.

Mwenyekiti wa CCM Dkt Jakaya Kikwete na Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana katika moja ya vikao vya Kamati Kuu ya CCM

Kamati kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imekutana mjini dodoma chini ya mwenyekiti wake Rais Jakaya Kikwete na kutoa tamko la kulaani kitendo cha wajumbe wa bunge maalum la katiba wanaounda kundi la umoja wa katiba ya wananchi (UKAWA) kususia vikao vya bunge hilo na kudai kuwa kundi hilo linakiuka katiba na halina nia wala dhamira ya kuhakikisha katiba mpya inapatikana.

Akitoa taarifa kuhusu kikao hicho cha dharura cha siku moja katibu wa itikadi na uenezi wa CCM Nape Nnauye amesema pamoja na mambo mengine kikao hicho kimepokea taarifa ya yaliyojiri ndani na nje ya bunge la katiba ambapo imesikitishwa na baadhi ya wajumbe wa bunge hilo kususia kikao hicho na kwenda kupotosha ukweli kwa wananchi wakati muda wa kupeleka rasimu ya katiba kwa wananchi bado haujafika.

Nape ameongeza kuwa CCM itaendelea kulinda maslahi ya nchi na kuhakikisha umoja na mshikamano wa nchi unadumishwa kwa gharama yeyote ile na itajibu kila uchochezi unaooneshwa na baadhi ya watu kwa maslahi yao binafisi kwa kuwaeleza watanzania ukweli.