Wednesday , 24th May , 2017

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli amemuomba Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo kujiuzulu nafasi yake kutokana na kushindwa kusimamia suala ya usafirishaji wa machanga nje nchi kwa manufaa ya taifa. 

Akizungumza baada ya kukabidhiwa ripoti ya matokeo ya uchunguzi wa mchanga wenye madini (makenikia) unaosafirishwa kwenda nje ya nchi, Rais Magufuli amesema viongozi wa wizara hiyo akiwemo waziri wameshindwa kutimiza majukumu yao ikiwemo ununuzi wa mashine ya uchenjuaji wa mchanga huo kama ambavyo sera ya madini inataka.

Sababu nyingine ni udanganyifu wa viwango na aina za madini yaliyomo katika mchanga huo, ambapo kamati hiyo imebaini viwango tofauti na vile vilivyoandikishwa na kutozwa kodi.

Mbali na waziri, Rais Magufuli pia amemsimamisha kazi Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Ukaguzi wa Madini (TMAA) pamoja na kuvunja bodi yake kutokana na kuhusika katika udanganyifu uliobainika pamoja na kushindwa kusimamia zoezi la upimaji, ukaguzi na uhakiki wa makontena yenye mchanga huo ambayo husafirishwa kwenda nje ya nchi.

Rais pia ameagiza vyombo vya dola ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kuwachunguza watendaji wote wanaohusika na mchakato wa usafirishwaji wa mchanga huo akiwemo kamishna wa madini aliyeondolewa kwenye nafasi hivi karibuni.

Rais Magufuli siku alipofanya ziara ya kushtukiza bandarini na kubaini uwepo wa makontena yenye mchanga wa madini 

Kamati hiyo imebaini kuwa kitendo cha kusafirishwa nje ya nchi kwa mchanga huo kimekuwa kikiliingizia taifa hasara kubwa kutokana na mchakato mzima kugubikwa na udanganyifu unaolisababishia taifa hasara kutokana na kutotoza kiwango sahihi cha mrabaha.

Pia kamati hiyo imebaini kuwemo kwa madini mengine kama vile Sulphur, Chuma, Nikel, Zinc n.k ndani ya mchanga huo ambayo huwa hayaingizwi katika hesabu na kukokotolewa tozo, madini hayo yamebainika kuwa na thamani ya kati ya shilingi bilioni 829.4 hadi trilion 1.43.

Takriban makontena 250 hadi 300 yenye mchanga huo husafirishwa nje ya nchi kila mwezi, ambapo kamati hii imefanya uchunguzi wake katika makontena 277 pekee.

Baadhi ya makontena yaliyokuwa bandarini tayari kwa kusafirishwa

Aidha kamati imekuja na mapendekezo 9 ikiwemo kuendelea kwa zuio la usafirishwaji wa mchanga huo, serikali kununua mtambo wa uchenjuaji wa mchanga huo ili zoezi hilo lifanyike nchini, serikali kuweka mfumo wa ushtukizaji katika mchakato wa usafirishwaji wa mchanga huo, mchanga wote wenye madini kupimwa na ili kubaini madini yote yaliyomo na thamani yake kabla ya usafirishwaji, n.k

Rais Magufuli amekubali mapendekezo yote yaliyotolewa na kamati hiyo iliyohusisha wataalam wa masuala ya madini na jiolojia kufanya uchunguzi.

Kamati hiyo iliyotoa matokeo yake leo ni moja kati ya kamati mbili alizounda, hivyo matokeo ya kamati nyingine inayohusisha wataalam wa uchumi inatarajiwa kutoa matokeo yake hivi karibuni