Thursday , 7th Aug , 2014

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa moja ya
sababu kubwa zinazokwamisha maendeleo makubwa zaidi na ya haraka zaidi ya Afrika ni uzalishaji mdogo na matumizi ya chini mno ya umeme.

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa hali hiyo inaeleza jinsi ongezeko la uzalishaji na matumizi ya umeme linavyoweza kuharakisha maendeleo ya Afrika na kuleta manufaa ya dhahiri kwa kila familia na kwa kila Mwafrika.

Rais Kikwete ameyasema hayo jana, Jumatano, Agosti 6, 2014, wakati alipozungumza kwenye Mkutano wa Kwanza wa Wakuu wa Nchi za Bara la Afrika uliofanyika chini ya uenyekiti wa Rais Barack Obama, ambaye ni mwenyeji wa Mkutano huo.

Rais Kikwete amewaambia wakuu wa nchi hizo kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kuwa ni dhahiri kuwa bila ongezeko kubwa la uzalishaji na matumizi ya umeme Bara la Afrika halitatoka kwenye uduni.

Rais amesema kuwa kwa mujibu wa Ripoti ya Kanda ya Shirika la Umoja wa Mataifa Mazingira (UNEP) “Efficient Lighting in Sub Saharan African Countries” matumizi ya umeme katika Bara zima la Afrika ni asilimia 31 tu na hivyo kulifanya Bara la Afrika kutumia asilimia tatu tu ya umeme wote duniani.

Rais Kikwete amesema kuwa ili kuelewa udogo wa matumizi ya umeme ya Bara la Afrika ni kuangalia matumizi ya nishani hiyo kwa kila mkazi wa Bara hilo na yule wa Marekani. Amesema kuwa wakati kila raia wa Marekani anatumia kilowati 13, 246 katika Afrika wastani ni kilowati 440.

Ameongeza Rais Kikwete: “Ukiondoa Afrika Kusini, matumizi ya umeme kwa kila raia wa Afrika yanateremka na kufikia kilowati 160 tu.”
Amefafanua Rais Kikwete: “Uzalishaji wa jumla wa umeme wa Bara la Afrika ni gigawati 63 ambazo ni sawa na umeme unaozalishwa na nchi moja tu ya Ulaya – Hispania. Ukiondoa Afrika Kusini, nchi zinazobakia wa Afrika zina uwezo wa kuzalisha gigawati 28 tu, kiasi ambacho kinazalishwa na nchi moja tu ya Marekani Kusini ya Argentina.”

Rais Kikwete ambaye alikuwa anafafanua jinsi utoaji huduma ulio dhahiri unavyoweza kunufaisha wananchi na kujenga mazingira ya taasisi zisizokuwa za kiserikali kushamiri, ametaja mambo mengine ya msingi ambayo ni lazima yawepo ili wananchi waweze kunufaika ikiwemo elimu, ushamiri wa sekta binafsi, sera sahihi za kiuchumi, uwekezaji katika ujenzi wa miundombinu na uboreshaji wa kilimo.

Pia Rais Kikwete ametaja mambo mengine muhimu yanayoweza kusaidia kuboresha maisha ya wananchi kuwa ni uendelezaji na matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano pamoja na kulea na kukuza demokrasia, utawala bora na utawala wa sheria.

Rais Kikwete ambaye yuko katika ziara ya kikazi ya siku tisa katika Marekani, anaondoka mjini Washington, D.C., leo kwenda Houston ambako atafungua na kushiriki katika mkutano wa uwekezaji katika uchumi wa Tanzania.