Tuesday , 26th May , 2015

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Rais wa Tanzania Dkt Jakaya Kikwete ameitisha mkutano wa dharura wa viongozi wa nchi za Afrika Mashariki kujadili hali tete ya kiusalama na mgogoro unaoendelea nchini Burundi, mkutano utakaofanyika Mei 31.

Marais wa nchi Tano zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo kwa sasa Mwenyekiti wao ni Dkt. Jakaya Kikwete wa Pili kushoto.

Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa Bernard Membe amesema hayo jijini Dar es Salaam jana usiku muda mfupi baada ya kupokea taarifa ya hali ilivyo nchini Burundi kutoka kwa mawaziri wa Afrika Mashariki waliopewa jukumu la kufuatilia mgogoro huo.

Kwa mujibu wa waziri Membe, hali ya nchini Burundi imezidi kuwa tete kiasi cha kutishia usalama wa mataifa jirani na nchi hiyo na kwamba juhudi za haraka zinahitajika katika kuutatua mgogoro huo.

Mbali ya marais wa nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika; viongozi wengine watakaohudhuria ni pamoja na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini, Jose Eduardo Dos Santos wa Angola, mwakilishi maalum wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, mwakilishi wa kamisheni ya nchi za maziwa makuu, Kamishna wa Umoja wa Afrika Bi. Nkosazana Zuma na wawakilishi wa vuguvugu la upinzani nchini Burundi.