Friday , 26th Dec , 2014

Wadau wa Uhifadhi wametakiwa kushirikisha jamii na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama katika mapambano ya kukomesha vitendo vya ujangiri wa tembo ili kuokoa wanyama hao katika hatari ya kutoweka.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Iringa Bw. Ramadhan Mungi.

Akifungua mkutano wa ushirikiano kati ya vyombo vya ulinzi na usalama na Jumuiya ya uhifadhi wa maliasili Mkoani Iringa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa Bw. Ramadhan Mungi amesema kukithiri kwa vitendo vya ujagiri wa tembo kunashusha heshima na hadhi ya doLa ya Tanzania katika Jumuiya za Kimataifa na kuonekana ni nchi ambayo haiwezi kusimamia na kulinda maliasili zake.

Kamanda Mungi ametaka kila raia wa Tanzania bila kujali nafasi aliyonayo katika jamii kuguswa na tatizo la mauaji ya tembo kwani kuendelea kwa vitendo hivyo kunadhalilisha jamii nzima ya Watanzania.

Naye Mratibu wa Mradi wa Kuendeleza maeneo yaliyohifadhiwa kusini mwa Tanzania Spanet, Bw. Godwel Ole Meing’ataki amesema mkutano huo umewakutanisha wadau hao ili kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha uhifadhi na ulinzi wa tembo na maliasili nyinginezo hapa nchini.