Monday , 21st Sep , 2015

Vijana wameitaka serikali ijayo kuboresha huduma za afya kwa kutenga bajeti kubwa kwa sekta ya afya, ili kuweza kutatua changamoto mbali mbali zinazoikabili sekta hiyo.

Rai hiyo imetolewa na Dokta Wilson Kitinya kutoka asasi ya kiraia ya Sikika, alipokuwa akiongea kwenye kipindi cha Super Mix kinachorushwa na East Africa Radio, na kusema kwamba iwapo serikali itaweka bajeti kubwa itaweza kupeleka madaktari kusoma, na hatimae kuwa na madaktari bingwa wa kutosha nchini.

Dkt. Kitinya ameongeza kwa kusema kwamba pamoja na hayo bajeti hiyo itaweza kulinda maslahi ya Madaktari na kupunguza vitendo vya rushwa, ambavyo vimekuwa tatizo kubwa kwa watu wanaohitaji huduma za afya, pamoja na kununua vifaa tiba na kusambazwa kwa wingi katika vituo vya afya, ili kutatua kero ya ukosekanaji wa vifaa tiba ikiwemo dawa, na kukidhi mahitaji ya jamii.

“Tatizo la rushwa kwa madaktari linasababishwa na ugumu wa maisha wanayokabiliana nayo madaktari, sasa iwapo serikali itatia mkazo na kuwaongezea bajeti, madaktari hawa hawatakuwa na tamaa za kuchukua rushwa kwa sababu mianya yote itakuwa imezibwa, kama vifaa na dawa zitakuwepo, na madaktari wakiwa wa kutosha, haitakuwa rahisi kwa rushwa kuwepo”, alisema Dkt. Kitinya.

Pia mmoja wa wadau waliotoa maoni kwenye kipindi hicho Dkt. Said Makame, ameshauri serikali kuboresha mfumo wa ugawaji dawa kwa kupeleka dawa hizo moja kwa moja kwenye vituo vya afya, na sikupitia bohari kuu ya dawa au halmashauri kama ilivyo sasa kwani itapunguza mlolongo wa upatikanaji dawa kwa urahisi kwenye vituo vya afya.