Monday , 23rd Jan , 2017

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, George Simbachawene ameeleza sababu zilikuwa zimekwamisha mikoa takriban saba kushindwa kutimiza malengo ya utekelezaji wa agizo la utengenezaji wa madawati.

Madawati

 

Simbachawene amesema amegundua tatizo kubwa lililosababisha kucheleweshwa kwa zoezi hilo ni kucheleweshwa kwa uteuzi katika nafasi mbalimbali, pamoja na mawasiliano mabovu katika safu za uongozi wa mikoa.

Waziri alikuwa akitoa maelezo kupitia kipindi cha Dakika 45 cha ITV kuhusu utekelezaji wa agizo lake alilotoa mwezi Novemba mwaka jana, ambapo alitoa muda hadi Januari 2017 mikoa hiyo iliyokuwa na upungu iwe imekamilisha zoezi hilo na kusema kuchelewa kwa uteuzi wa makatibu tawala na wakurugenzi kumechangia kwa kiasi kikubwa mipango mingi kutofanyika kwa wakati ikiwemo hiyo ya madawati.

"Sababu kubwa ni mawasiliano, lakini nadhani kuchelewa kwa uteuzi wa nafasi mbalimbali hususani wakurugenzi wa halmashauri kumechangia, tunashukuru wakurugenzi wapya ni waaminifu sana na waadilifu, wanachapa kazi, matokeo ni mazuri, wamejitahidi, madawati yanawekwa na ukarabati wa madarasa pia umefanyika" Amesema Simbachane.

Mikoa iliyokuwa imepewa muda huo, na wakuu wake kuelezwa kuwa ni pamoja na mkoa wa Geita, Mwanza, Kigoma, Mara, Dodoma, Rukwa na Simiyu.

Waziri George Simbachawene

Pia amekiri uwepo wa upungufu wa vyumba vya madarasa ambapo amesema kuwa baada ya zoezi la madawati kukamilika, sasa nguvu zinahamia kwenye vyumba vya madarasa.

"Bilioni 25 kila mwezi inakwenda kwa ajili ya elimu msingi, tunakiri madarasa ni changamoto kwa sasa na huko ndiko nguvu zetu zinahamia kwa sasa, Tumefanya kazi kubwa sana, yaani ndani ya mwaka mmoja kumaliza tatizo la madawati ni kazi kubwa, tukifunga hilo zoezi, nitawatangazia wadau jinsi tulivyofanikiwa"