Wednesday , 17th Oct , 2018

Takribani wanafunzi 14 762 waliokosa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu nchini wamepewa nafasi ya kukata rufaa ya kuomba tena kwa ajili ya awamu zinazofuata.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo (HESLB), Abdulrazaq Badru

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu nchini (HELSB), Abdulrazaq Badru, amesema wamepokea maombi mapya ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza 40,285, ambapo wanafunzi 25,532 kati yao wametajwa kukidhi uhitaji wa mikopo kwa awamu ya kwanza. Kati yao zaidi ya wanafunzi elfu 16 ni wakiume na wanafunzi wakike elfu 9.

Jumla ya wanafunzi 25,532 wa mwaka wa kwanza wamepangiwa mikopo, mikopo hiyo inathamani ya bilioni 88.36 na tumeangalia jinsia kwenye utoaji wa mikopo”, amesema.

Aidha Mkurugenzi huyo amesema HELSB itakuja na awamu ya pili ya utoaji wa mikopo kwa wanafunzi ambao hawakupata mikopo kwenye awamu ya kwanza kabla ya vyuo havijafunguliwa.

Katika hatua nyingine Badru amesema bajeti ya fedha za mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2018/2019 ni Shilingi bilioni 427.5 na tayari serikali imeshatoa kiasi cha Shilingi bilioni 137.06 kwa ajili ya kuwakopesha wanafunzi wapya 123,285.