
Lipumba ametoa kauli hiyo leo, jijini Dar es salaam wakati akizungumza na wanahabari, ambapo amesema kuwa endapo watafanyiwa hujuma kwenye uchaguzi wa Liwale, wanachama wake hawatokubali kwakile alichodai kuwa jimbo hilo ni ngome ya CUF.
"Hivi kweli CCM na serikali wanataka tuomboleze kifo cha Baba wa Taifa kwa maafa ya Liwale jimbo lililokuwa la Kawawa, namuuliza kijana wangu Bashiru Ally je hii ndio njia sahihi ya kumuenzi Mwalimu Nyerere maana Uchaguzi ni tarehe 13 na oktoba 14 siku ya Mwalimu Nyerere, hebu wajipime, kata walizoshinda ni kata tatu tu kwenye uchaguzi wa 2015", amesema Profesa Lipumba.
Miongoni mwa malalamiko ya awali aliyoyayatoa Lipumba, ni kucheleweshwa kwa hati ya uapisho kwa baadhi ya mawakala wa Uchaguzi, kuenguliwa kwa mgombea udiwani kwa madai ya kutolipa fedha fomu ya udiwani, pamoja na kukamatwa kwa mawakala wake.
"Tunatoa wito kwa Tume ya Uchaguzi kuhakikisha mawakala wetu wanakuwa kwenye vituo na wanapewa nakala za matokeo, na tunaiomba Serikali kutumia busara, maana wamefanya makosa kumteua Kachauka kugombea Liwale", amesema Lipumba.