Friday , 18th Nov , 2016

Hospitali zote za umma jijini Dar es Salaam hivi karibuni zitaanza kutumia panya kwa ajili ya kupima sampuli za ugonjwa wa kifua kikuu.

Mtaalam wa maabara akitumia panya kupima sampuli za ugonjwa wa kifua kikuu

Panya hao ni wale waliopewa mafunzo maalum mafunzo maalum ya kutambua ugonjwa huo hatua ambayo imeelezwa kuwa itasaidia kupunguza maambukizi na kurahisisha tiba za ugonjwa huo.

Panya hao ni wale wanaotokana na mradi wa Apopo TB Programme ulio chini ya Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine kilichopo mkoani Morogoro, ambapo kwa mujibu wa Meneja Mradi wake Dkt. Georgies Mgode tayari maabara ipo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupima sampuli zote za kifua kikuu.

Kwa mujibu wa Dkt Mgode, zaidi ya hospitali 20 zimeshafanya majaribio ya kutumia panya hao katika kupima makohozi yanayohofiwa kuwa na vijidudu vya ugonjwa wa kifua kikuu na kwamba panya hao hutumia muda usiozidi dakika moja kubaini iwapo makohozi yana vijidudu vya kifua kikuu na kwamba hiyo ndiyo teknolojia pekee iliyopo duniani kwa sasa inayopima kifua kikuu kwa haraka zaidi.

"Mwongozo wa Shirika la Afya Ulimwenguni WHO unaelekeza kuwa kila mtaalam wa maabara anatakiwa apime sampuli zisizozidi 60 kwa siku lakini kutokana na wingi wa sampuli za magonjwa mbalimbali, wataalam hao wamejikuta hawafikii lengo hilo na hivyo kufanya muda wa kusubiri majibu ya vipimo vya kifua kikuu kuchukua muda mrefu, "amesema Dkt Mgode.

Ameongeza kuwa "Katika kipindi cha kusubiri majibu, wagonja wengi hupoteza maisha na maambukizi mapya kutokea na kwamba kwa kutumia panya hao vifo na maambukizi ya kifua kikuu kwa ujumla yatapungua".

Kuhusu utaratibu mzima wa kupima kifua kikuu; Dkt. Mgode amesema kila hospitali itakuwa ikipeleka sampuli hizo katika maabara hiyo na kwamba kwa kutumia panya, muda wa vipimo utapungua kutoka wastani wa siku tano za sasa hadi siku moja.